Wiki moja au mbili zilizopita nilipokuwa mtandaoni niliona kuwa Julius Malema, mmoja wa wabunge katika nchi ya Afrika Kusini, alikuwa amesema ya kwamba ingekuwa vyema kama Afrika ingekuwa na lugha moja inayotuunganisha sisi sote. Siyo kwamba alikuwa anataka tuache lugha zote tunazozizungumza—kwa kuwa kuna lugha nyingi ambazo zinazungumzwa Afrika—lakini alikuwa anataka lugha moja iwe lingua franca yetu, na akataja kuwa angependa lugha hiyo iwe Kiswahili. Tena leo nilipokuwa mtandaoni nikaona kuwa Afrika Kusini imeamua kuwa lugha ya Kiswahili itafunzwa katika shule zao. Hip hip hoyee! Furaha iliyoje? Ningetaka kuyajua maoni yenu kuhusu suala hilo.
0 Comments
9/9/2018 0 Comments UTANGULIZIHabari zenu na karibuni katika ukurasa huu mpya kwenye tovuti yangu. Kama umekuwa ukinifuata kwa muda sasa, unajua kuwa tovuti hii huwa katika lugha ya Kiingereza. Nilipokuwa nimekaa nyumbani mwangu nikiwaza, nilijiuliza kwa nini wengi wetu ambao twazungumza lugha ya Kiswahili huwa hatushughuliki kuitumia lugha hii katika shughuli zetu za mtandaoni. Najua kwamba watu wengi hawakielewi Kiswahili huko nje, lakini shida ni kwamba wengi wetu humu Afrika Mashariki tumeanza kukisahau Kiswahili pia. Kuna watoto wengi wa siku hizi ambao wanafikiria kuwa Kiswahili ni lugha mbovu, lugha ya shida, lugha isiyofahamika mbele wala nyuma. Kuna watu kati yetu walio na pesa na ambao wametembea humu duniani ambao wamekiacha Kiswahili kwa sababu wanafikiria kuwa lugha za wazungu ndizo mwanzo tena mwisho. Hiyo ndiyo maana nimeamua kuwa nitaanza kuandika hapa kwa Kiswahili. Ingawaje, kwa kuwa maswala mengi huwa tunayazungumzia kwa Kiingereza, unawezapata kuwa Kiswahili changu kinaweza kuwa hivi hivi tu, haswa katika maswala ya sayansi, lakini natarajia ya kwamba nitajijenga na msamiati wangu utaongezeka. Nitafurahia sana mkijiunga nami katika safari hii ya kukiimarisha Kiswahili. Ningependa kumalizia kama vile tulivyokuwa tukimalizia insha zetu katika shule za msingi: kama wahenga walivyosema, "Tukijenge Kiswahili kwa uti na umbari, kwa kuwa ni lugha ya taifa."
|
AboutCreated with the aim of encouraging people to speak Kiswahili. ArchivesCategories |